Ijumaa , 11th Jun , 2021

Kituo namba moja kwa vijana nchini cha East Africa Television na East Africa Radio vimeingia makubaliano na Taasisi ya Flaviana Matata Foundation (FMF) kushirikiana katika kampeni ya Namthamini kwa mwaka 2021 katika kufanikisha kupatikana kwa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa EATV na EA Radio Regina Mengi na Muasisi wa Taasisi ya Flaviana Matata Foundation Flaviana Matata wakitia saini makubaliano ya ushirikiano kwa ajili ya kampeni ya Namthamini ya mwaka 2021

Makubaliano hayo yamefanyika leo Juni 11, 2021 na kutiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa EATV na East Africa Radio, Regina Mengi na Muasisi wa Taasisi ya Flaviana Matata Foundation, Flaviana Matata, katika hafla iliyofanyika ofisi za EATV na East Africa Radio zilizopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

Awali akizungumza katika zoezi hilo Mwakilishi wa EATV na Radio Sophia Proches amesema ushirikiano baina ya Namthamini na Taasisi ya FMF utasaidia kuongeza nguvu ya upatikanaji wa taulo za kike pamoja na kuhamasisha wadau wengine zaidi kujitokeza kumchangia ili kumasaidia mtoto wa kike.

"EATV na East Africa Radio tangu tumezindua kampeni hii ya Namthamini 2017, tumefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanafunzi 11,000 katika mikoa zaidi ya 15 nchini na kupawatia taulo za kike za kujistiri, tunapenda kuchukua nafasi hii kuomba Watanzania wote kushirikiana nasi katika kampeni hii kwa kuchangia taulo za kike ili mtoto wa kikea apate elimu bila vikwazo vyovyote na kufikia malengo yake" amesema Sophia. 

Naye Muasisi wa Taasisi ya Flaviana Matata Foundation, Flaviana Matata ametoa shukrani kwa EATV na East Africa Radio kwa kampeni hii na kueleza kuwa wamepanga kuwafikia wanafunzi wa kike elfu tano kwa mwaka huu huku akitoa rai kwa wadau wengine ikiwemo vyombo vya habari kushirikiana katika kampeni hii ili kuwafikia watoto wengi zaidi.

"Nipende kutoa shukrani zangu kwenu kwani tunajua changamoto ni nyingi zinazomzuia mtoto wa kike kwenda shule kutokana na kutomudu gharama za taulo za kike na kwa kushirikiana tumepanga kufikia watoto elfu tano mwaka huu," amesema Flaviana.

EATV NA East Africa Radio imezindua kampeni yake ya Namthamini mwaka 2021 na kuwaalika wadau na Watanzani kushiriki kwa pamoja katika kuchangia taulo za kike ili kumtoa hofu mwanafunzi wa kike ya kukosa masomo kwa sababu ya hedhi. 

Unaweza kuchangia kampeni hii kwa kutuma michango wako kwa MASTERPASS namba 6057 9851, jina NAMTHAMINI au kuwasilisha moja kwa moja mchango wako ofisi zetu za EATV na East Africa Radio zilizopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam.