Jumanne , 2nd Jul , 2019

Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, ameshangazwa na hatua ya Spika wa Bunge Job Ndugai,  kumvua ubunge wa Singida Masharika Mh Tundu Lissu, siku ya Juni 28 mwaka huu.

Bernard Membe

Membe ameyasema hayo leo Julai 2 nje ya Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Dar Es Salaam,  ambapo amesema anao uhakika kwamba, Lissu atakaporudi ataenda mahakamani na kama kuna haki ataipata.

Aidha Membe amezungumzia suala la utekaji linaloendelea hapa nchini,  ambapo amewataka viongozi wa serikali na Chama kulikemea jambo hili.

''Mimi naona huu ni utamaduni mpya ambao haukubariki, na ningependa kuchukua nafasi hii kusema tu kwamba,  suala la utekaji ama watu kupotea linaweza kuiharibia nchi yetu heshima duniani'', amesema.

 Ameongeza, ''ningependa kuwaomba viongozi wa chama na serikali kulifikiria suala hili kulikemea jambo hili ili lisitokee, tujifikirie sisi wenyewe kama watoto wetu wakitekwa, wenzetu wa dunia watashindwa kuja kutalii''

Amemaliza kwa kusema hatuwezi kuendelea kukaa  kwenye nchi ya watu wenye wasiwasi na uoga wasiojua kesho wataamuka vipi na hii ajenda iishe maana isipoisha itaenda mwapa kwenye uchaguzi.