
Mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Manyara imemuhukumu Hamis Abdalah mwenye miaka 42 mkazi wa Babati Manyara miaka sita jela na faini ya milioni moja baada ya kutiwa hatiani na kosa la kujeruhi kwa kumkata masikio mtoto wa jirani yake mwenye umri wa miaka 13 aliyeelezwa kwamba alimuibia yai moja la kuku.
Hukumu hiyo imesomwa mbele ya hakimu mkazi mkoa wa Manyara Martini Masao, ambapo mshitakiwa huyo ameelezwa kutenda kosa hilo mnamo 23.08.2025.
Kesi hiyo namba 23254 ya mwaka 2025 imetolewa hukumu hii leo kwenye mahakama hiyo ya hakimu mkazi mkoa wa Manyara, ambapo mshtakiwa huyo Hamis Abdala alimkata masikio yote mawili kwa kutumia kiwembe, kumchanja kifuani pamoja na kumbamiza kichwa ukutani.
Mbele ya mahakama Hakimu Martin Masao alimuuliza mshtamiwa huyo unachochote cha kuiambia Mahakama? mshtakiwa huyo aliijibu mahakama "SINA CHOCHOTE" cha kuiambia mahakama.
Mara baada ya mshtakiwa huyo kudai hana chochote cha kuiambia mahakama ndipo Hakimu Martin Masao alipotoa hukumu hiyo kwa mshtakiwa kwenda jela miaka sita na faini ya milioni moja.
Hata hivyo Hakimu Martin Masao aliiambia mahakama kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 225 cha kanuni za adhabu kwa makosa ya jinai sura ya 16 marejeo 2023.