Jumatatu , 15th Jul , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemuagiza Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, kuhakikisha anafuatilia malipo yote ambayo Serikali inatakiwa kulipa Nchini India.

Rais Magufuli

Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Julai 15, wakati wa shughuli ya uzinduzi wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, ambapo amesema lengo la kufanya hivyo, ni kudhibiti  vizuri matumizi ya watu wanaotibiwa India ilihali hawana magonjwa ya kuwapeleka huko.

''Wapo watu hapa waliokuwa wanapewa vibali kwenda kutibiwa India kumbe wanaumwa mafua, Mh Waziri  wa Afya akafuatilie malipo tunayotakiwa kulipa India, ukikuta kuna mtu alitibiwa wakati hakuwa mgonjwa akazilipe mwenyewe, lazima tujenge nidhamu ya nchi yetu'' amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa, Serikali haikatai watu kwenda kutibiwa nje, lakini iwe ni kwa magonjwa, ambayo yameshindikana kutibika hapa nchini.

Rais Magufuli pia imeitaka Wizara ya Afya, kuhakikisha lazima inapata ufumbuzi wa kweli, ili kubaini nini chanzo na sababu inayopelekea, wananchi na wakazi wa kanda ya Ziwa kuongoza  kwa kuumwa ugonjwa wa Saratani.