Jumatatu , 22nd Jun , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuonya Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Jonathan Shana kutokana na kufanya mambo ambayo hayapo kwenye kazi yake.

Rais Magufuli na Kamanda Polisi mkoani Arusha, Jonathan Shana

Amesema hayo leo Juni 22, Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali wateule ambapo amesema kuwa ameamua kumsamehe Kamanda Shana pamoja na Afisa wa TAKUKURU mkoani humo lakini wasifanye makosa.

"IGP na Mkurugenzi wa TAKUKURU mko hapa, mkawaambie watendaji wenu walioko Arusha wafanye kazi nilizowatuma, nao leo nilikuwa niwatoe ambao ni RPC na Mkuu wa TAKUKURU wa Arusha", amesema Rais Magufuli.

"Nimeamua kuwasamehe lakini sijawasamehe moja kwa moja wakifanya kosa lolote wataondoka. Wakafanye kazi nilizowatuma wasifanye kazi wanazojituma wao, haiwezekani watu umewatuma kufanya kazi za serikali wanafanya kazi wanazozijua wao", ameongeza.

Katika tukio hilo, Rais Magufuli amemuapisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha mteule, Idd Kimanta pamoja na kushuhudia uapisho wa wakuu wawili wa wilaya ya Monduli, ACP Jotham Balele na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa.

Tazama tukio zima hapa.