Jumamosi , 25th Oct , 2014

Chama Cha Ukombozi wa Umma CHAUMMA, leo kimeibua mapungufu na kasoro kubwa kwenye Katiba Inayopendekezwa, kwa kile ilichoeleza kuwa Katiba hiyo imewanyima wananchi wa Zanzibar haki ya kutoa mgombea wa kiti cha nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma - CHAUMMA Bw. Hashim Rungwe Spunda (kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Ali Omar Juma (mwenye shati jeupe) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo.

Chama Cha Ukombozi wa Umma CHAUMMA, leo kimeibua mapungufu na kasoro kubwa kwenye Katiba Inayopendekezwa, kwa kile ilichoeleza kuwa Katiba hiyo imewanyima wananchi wa Zanzibar haki ya kutoa mgombea wa kiti cha nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Ali Omar Juma amesema hayo leo wakati wa mkutano wa Kamati Kuu ya cham hicho ambayo pamoja na mambo mengine inajadili mwelekeo wa kisiasa nchini na hasa mustakabali wa mchakato unaoendelea wa kutafuta katiba mpya.

Akisoma tamko kwa niaba ya mwenyekiti wa chama hicho Bw. Hashim Rungwe Spunda; Bw. Juma amesema CHAUMMA inapinga kwa nguvu zote katiba inayopendekezwa kwa madai kuwa imeacha maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo mwenyekiti wake alikuwa Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.

Kwa mujibu wa Bw. Juma, chama hicho kinakusudia kwenda mahakamani kufungua shauri ambapo kitaitaka mahakama itoe Tafsiri ya Kisheria na ya Kikatiba, juu ya mamlaka ya lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, katika kubadilisha mambo ya msingi yaliyomo katika mkataba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mambo hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa misingi ya yaliyokuwa makubaliano ya Muungano yanalindwa na kuheshimiwa, moja ya makubaliano hayo ni pamoja na kuwepo kwa ushiriki sawa wa kiuongozi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulingana na sheria na taratibu za kimataifa zinazosimamia muungano wa nchi mbili zenye mamlaka kamili.

Hatua hiyo ya CHAUMMA imeamsha kelele mpya na hoja za msingi zinazotolewa na wadau wa mchakato wa katiba, ambao kwa siku kadhaa sasa wamekuwa wakipinga katiba inayopendekezwa kwa madai kuwa imeacha hoja za msingi za wananchi na kuweka zile walizodai kuwa zina maslahi kwa chama tawala CCM.

Aidha, katika hatua nyingine, Bw. Juma amepongeza na kusifu juhudi zinazofanywa na Watanzania wachache akiwemo Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dkt Reginald Mengi, za kuamua kutumia akili na rasilimali chache walizojaliwa na Mwenyezi Mungu, kuwekeza nchini na kuanzisha vitega uchumi ambavyo vimeajiri na kuwa msaada mkubwa wa watanzania maskini.

Amesema tofauti na wawekezaji toka nje ambao mara nyingi serikali imekuwa ikiwakumbatia, wawekezaji wazawa kama Dkt Mengi ni hazina kwa taifa kwani kila wanachokipata kinabaki hapa nchini na kuwasaidia watanzania wenzao badala ya wawekezaji wa kigeni ambao mapato ya uwekezaji wao wanayahamisha kama faida na kwenda kunufaisha ndugu zao huko ughaibuni.

Katibu Mkuu huyo wa CHAUMMA amesema ni jukumu la serikali sasa kuhakikisha wawekezaji wazawa kama Dkt Mengi wanawezeshwa na kupewa kila aina ya msaada wanaouhitaji kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamewainua kiuchumi idadi kubwa ya Watanzania.

Mbali ya kuwainua wawekezaji wazawa, CHAUMMA imeitaka serikali kuboresha mfumo wa elimu na kuja na mfumo mpya ambao utasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kupunguza kiwango cha umaskini unaowakabili Watanzania wengi.