Jumanne , 17th Jan , 2023

Jovitus Kazimoto (38) mkazi wa Nyamhongolo manispaa ya Ilemela jijini Mwanza amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza kwa tuhuma za kuingiza nchini mifuko ya plastiki iliyokatazwa.

Mshtakiwa huyo amesomewa shtaka lake na mwendesha mashtaka wa serikali Sabina Chongolo mbele ya hakimu mkazi Bonaventure Lema ambapo inadaiwa kuwa mnamo Desemba 16/2022 mshtakiwa huyo aliingiza nchini mifuko ya plastiki ambayo imekatazwa na serikali kinyume na kifungu cha 8 cha sheria ya uhifadhi wa mazingira na kanuni za mwaka 2019 zikisomwa pamoja na kifungu cha 230 ya sheria ya uhifadhi wa mazingira sura namba 191

Aidha mwendesha mashtaka huyo wa serikali Sabina Chongolo amesema mshtakiwa huyo alikamatwa na jeshi la polisi wilayani Sengerema akiwa na shehena ya mifuko hiyo ya plastiki viroba 45 vikiwa kwenye gari lenye namba za usajili T.421 ADM Mitsubish canter akiwa anaisafirisha

Baada ya kusomewa shtaka lake la kuingiza nchini mifuko ya plastiki iliyokatazwa na serikali mshtakiwa huyo ajulikanaye kama Jovitus Kazimoto alikana shtaka hilo ndipo mahakama ikasema dhamana ya kesi hiyo iko wazi ambapo mshtakiwa huyo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao walitakiwa kusaini bondi ya shilingi milioni tano kila mtu

Baada ya mhakama kutoa masharti hayo ya dhamana mshtakiwa huyo alifanikiwa kudhaminiwa na hakimu Lema akaiahirisha kesi hiyo hadi tarehe 30 ya mwezi huu itakapotajwa tena