Alhamisi , 19th Mar , 2015

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania-LHRC kimewataka viongozi waheshimu Katiba na kuitaka sekretarieti ya maadili ya viongozi kusimamia maadili ya viongozi licha ya Katiba mpya kukosa vipengele muhimu ikiwemo kile kinachohusu maadili.

Mkurugenzi wa Utetezi wa LHRC Bw Harold Sungusia (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa uwezeshaji Bi. Emelda Urio (katikati).

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa uwezeshaji wa (LHRC) Bi. Emelda Urio amesema Katiba inayopendekezwa ina mapungufu mengi na kuwataka wananchi waweze kuisoma Katiba hiyo na kuwataka kuwa makini katika kutoa maamuzi ya upigaji kura kwa kuzingatia mambo muhimu yanayohusu utetezi wa haki zao.

Aidha, Bi Urio amewataka waandishi wa habari nchini kutumia nafasi zao katika kutoa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya Katiba iliyopendekezwa na kutaka kuwepo na utekelezaji wa sheria ya maadili ya viongozi ya umma ikiwemo kuwajibishwa kutokana na kauli wanazotoa kwa umma.

Hata hivyo amesema viongozi wamekuwa wakiwarubuni wananchi wakati wa kuomba kura na pindi wanapopatiwa nafasi za uongozi husahau kutimiza ahadi alizotoa na hivyo katiba ya sasa inashindwa kutoa makali kwa wananchi kuwawajibisha viongozi hao.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Utetezi wa LHRC Bw Harold Sungusia amesema kumekuwepo na mkanganyiko katika utoaji wa adhabu na tume ya maadili kutokana na kuwepo kwa muingiliano baina yake na upande wa mahakama.