Jumapili , 20th Jan , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, amedai kushangazwa na kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu kutumia nafasi yake ya Ustaafu wa Urais wa Chama cha Wanasheria kuwashawishi mawakili wajitoee katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Kulia pichani ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kushoto.

Katika waraka aliouandika kupitia ukurasa wake wa Instagram, Paul Makonda amedai kwamba alitegemea baada ya Lissu kupona angerejea nchini ili kumsaidia Mbowe katika kesi na siyo kufanya ziara katika nchi za Ulaya kama afanyavyo sasa.

"Tulitegemea wewe kama Mwanasheria ungekuwa umerejea nchini na kumsaidia mbowe lakini uroho wa madaraka umekufanya kutumia matatizo yake kujiimarisha kisiasa na kutafuta uraisi", ameandika Makonda.

Makonda ameongeza kwamba, "Mbaya zaidi unajua Mwenyekiti wa chama ambaye kimsingi ndiye aliyekupigania kutafuta fedha, kukaa na wewe Nairobi na kuja mpaka Ubeligiji umeamua kumwacha ateseke na kutumia nafasi yako ya Urais ustaafu wa TLS kuwashawishi Mawakili wajitoe ili aendelee kuteseka huku wewe ukitumia fursa hii kutafuta uraisi. Hauangaiki wala hata haufikirii kwamba ni wakati muafaka kurudi kuja kumpa moyo kama ambavyo alifanya yeye. Kweli hayo ndio malipo unayompa Mbowe kwa kukuangaikia wewe upate matibabu bora".

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki amenza ziara yake katika nchi za Ulaya ambapo amesema ataeleza kile ambacho kilichomtokea Septemba 07,2017 maeneo ya nyumbani kwake area D kwa kupigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana alipokuwa akitoka kwenye vikao vya bunge.

Hivi karibuni Lissu alipokuwa akizungumza na Shirika la Utangazaji la BBC, alisema endapo chama chake kitampa baraka ya kuwania nafasi ya urais 2020 yeye yupo tayari.