
Rais John Magufuli
Mapema mwezi Machi mwaka huu Serikali ya Tanzania ilikubali ombi la Kenya la kuisaidia nchi hiyo madaktari 500 watakaosaidia kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba kufuatia kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo.
Hatua hiyo ya kuwaajiri madaktari hao imefikiwa na Serikali baada ya baadhi ya madaktari nchini Kenya kuwasilisha pingamizi mahakamani kuitaka serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri madaktari 500 kutoka Tanzania ambao waliombwa na nchi ya Kenya.
Akizungumza leo na waandishi wa Habari Bungeni mjini Dodoma,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema,kufuatia uamuzi huo,majina ya madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya Wizara hiyo.
Waziri wa Afya - Ummy Mwalimu
Amesema kuwa Rais amefikia uamuzi huo baada ya mahakama nchini Kenya kuweka pingamizi hilo serikali ya Tanzania, imeamua madaktari hao ambao walionesha utayari wa kufanya kazi katika mazingira yoyote waatiwe ajira hapa nchini badala ya nchini Kenya kama ilivyokuwa hapo awali.
Aidha Waziri Mwalimu ameongeza kuwa wizara ilipokea maombi 496 na baada ya kuyachambua madaktari 258 ndiyo waliokidhi vigezo vilivyokuwa vimewekwa, pamoja na hayo amesema kuwa bado Tanzania ipo tayari kuipatia nchi ya Kenya madaktari wengine pindi wakiwahitaji.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko juu ya upungufu wa wataalam wa afya katika vituo vya afya hasa katika vituo vya afya vilivyoko maeneo ya vijijini hivyo kuajiriwa kwa madaktari 258 kutasaidia kupunguza tatizo hilo.
Wakati huo huo katibu mkuu wizara ya afya Dkt. Mpoki Ulisubisya amewatoa hofu watanzania juu ya ugonjwa wa hamofilia kwa kusema kuwa ugonjwa huo si wa ajabu na mpya kama wengi wanavyodhani bali ni ugonjwa wa hatari kwani ni wa kurithi ambao husababisha shida katika damu kuganda na kuwa wapo wataalum wengi amabao wanaweza kushughulikia tatizo hilo.