Jumatatu , 29th Feb , 2016

Watanzania wengi wameonekana kutokuwa na uelewa juu ya magonjwa yasiyotambulika hali inayopelekea kuhusisha magonjwa hayo na imani za kishirikina hasa mara baada ya kuambiwa na daktari kuwa ugonjwa hauonekani na kupelekea taharuki kubwa kwa wauguzi.

Mtaalam wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Kareem Manji amesema kuwa magonjwa yasiyotambulika yamekuwa tishio na yanawaathiri watu wengi ambao hawajui wanasumbuliwa na maradhi gani ikiwa ni pamoja na kuyagundua mapema na kukabiliana nayo kitiba.

Profesa Kareem ametoa wito huo leo jijini Dar es salaam ikiwa ni siku ya maadhimisho ya magonjwa yasiyotambulika duniani na kuongeza kuwa enzi za zamani magonjwa mengi yalihusishwa na imani za kishirikina na kuwapa wagonjwa matibabu yasiyoendana na tatizo na hivyo kuchelewesha upatikanaji wa tiba kwa haraka.

Aidha kwa upande wake daktari wa watoto wa hospitali ya Aghakan Mariam Noorah amesema kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha linaweka mazingira mazuri ya tiba kwa ajili ya watoto watakaozaliwa wakiwa na tatizo la maradhi hayo na jamii ipate uelewa kuwa kati ya watoto 2,500 wanaozaliwa mmoja huwa na tatizo la ugonjwa usiotambulika ambapo mengi ya magonjwa hayo huwa kwenye moyo, ubongo, ini, figo, na Mapafu.

Wazazi wanaohudumia watoto wenye maradhi haya wamesema kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa vipimo sahihi kwa wagonjwa hali inayopelekea daktari kusema haoni ugonjwa wowote kwa mtoto na kupelekea taharuki juu ya kinachomsumbua mgonjwa, Aidha wameshauri serikali kutenga shule maalum za kuwasaidia watoto hao.