Jumapili , 2nd Feb , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha jana Februari 1, 2020, wakati wakikimbilia kukanyaga mafuta ya upako katika kongamano la Mtume Boniface Mwamposa, mkoani Kilimanjaro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Salamu hizo amezituma leo Februari 2, 2020, pamoja na kutuma salamu za pole na rambirambi kwa familia za watu zaidi ya 20 waliopoteza maisha mkoani Lindi, kutokana na madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

"Watu 20 waliopoteza maisha Moshi ni miongoni mwa wale waliohudhuria ibada ya Mtume Boniface Mwamposa na wamefariki baada ya kukanyagwa na wenzao wakati wakitoka kwenye lango moja waliloelekezwa kukanyaga mafuta ya upako, watu 16 pia wamejeruhiwa katika tukio hilo" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote kuchukua tahadhari kwenye matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko ya watu na mvua zinazoendelea, kwani amesikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo.