Jumatatu , 29th Jul , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda, leo Julai 29 amezindua kampeni ya tano ya usafi yenye lengo la kuendeleza kufanya usafi kwa jiji hilo ikiwa ni hatua za maandalizi ya kupokea ugeni wa viongozi wa SADC.

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda

Katika hotuba yake Makonda amewataka wakazi wa Dar Es Salaam, kuzingatia usafi na kupiga marufuku mtu yoyote kufika mjini kama hajafanya usafi wa mwili wake ikiwemo kuoga, kufua na kupiga pasi nguo zake.

“Tabia ya kuja mjini hujafua, hujaoga usitutie aibu kama umezoea kuja mjini hujaoga wala kufua nguo baki nyumbani walau huu mwezi wa nane uishe, tunataka sio usafi tu wa mazingira, usafi pia wa wananchi wetu, watu wamejaa chawa tu hapa”. Amesema.

Aidha Makonda amehimiza suala la usafi na kuwaagiza wanajeshi na wanamigambo waliosambazwa kwa ajili ya kufanya usafi wa jiji, kuhakikisha wanamchukulia hatua dereva wa gari binafsi atakayetupa taka hovyo.

“Ule utaratibu wetu wa Lugalo tunauanza rasmi leo haiwezekani wawe na nidhamu kwenye kile kipande cha kukaribia mita 200, 300 kwahiyo ule utaratibu wa mtu kwenye gari kutupa taka hovyo mshusheni akikataa chukueni namba yake ya gari tutamkamata ili aje apige deki” Amesema Makonda.

Takribani vijana 430 wa Jeshi la kujenga Taifa pamoja na wanamigambo wamesambazwa katika jiji la Dar Es Salaam kwa ajili ya zoezi la kufanya usafi.