
Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya, Aminiel Aligaesha
“Hivi karibuni, TANNA ilitoa maoni yake kuhusu tukio la video iliyosambaa kwenye kwenye mitandao ya kijamii na kuzua taharuki ikiwahusisha Rose Shirima (Muuguzi & Mkunga) na James Chuchu (Mteknolojia Maabara) Watumishi wa Zahanati ya Ishihimulwa, Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora ambao walikua wakijibizana (bila staha) kuhusu matumizi ya kipimo cha haraka cha kupima malaria (MRDT) kinachodaiwa kuisha muda wake”
“Taarifa ya TANNA ni maoni yao , Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI inapenda kuwafahamisha umma kuwa zilituma Timu ya Wataalamu kuchunguza tukio hilo tangu lilipotokea na uchunguzi wa suala hili bado unaendelea”
“Mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI zitatoa taarifa rasmi kwa umma baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi, Wizara inawaomba Wananchi kusubiri taarifa hiyo kutoka kwenye vyombo vyake”
Itakumbukwa uchunguzi wa TANNA ulibaini uwepo migogoro binafsi ya muda mrefu baina ya wawili hao na kwamba kabla ya kuanza kurekodi video kulikuwepo na lugha za matusi kutoka kwa James kwenda kwa Rose pia ulibaini alichokisimamia Rose kilikuwa sahihi.