Jumatano , 17th Feb , 2021

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa ameshtushwa na taarifa za kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, kilichotokea hii leo na kutoa pole kwa familia yake.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe

Mbowe ameyaandika hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, masaa kadhaa tu tangu kifo cha Maalim Seif, kitangazwe na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi.

"Nikiwa hapa Dubai, UAE, nimeshtushwa na taarifa za kutwaliwa kwa Mhe. Sharif Hamad, jabali la mageuzi Tanzania, Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, natoa pole nyingi kwa familia, chama chake, Wazanzibari na Watanzania wote, kwake tumetoka na kwake tutarejea. Amin", ameandika Mbowe.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameandika kuwa, "Mh Maalim Seif, alikuja kunisalimia nilipokuwa mahabusu, alinitia moyo, aliniambia mawazo imara na fikra thabiti juu ya ukombozi yana patikana jela, alinieleza kwa kifupi safari yake ndani ya magereza enzi zake, ninawapa pole familia na chama chake,tuchuke tahadhari Corona inaua".