Jumamosi , 15th Dec , 2018

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi Gibson Meseyeki amelalamikia namna ambavyo viongozi wa wilaya yake walimpokea Rais John Pombe Magufuli kwenye jimbo lake mkoani Arusha, licha ya yeye mwenyewe kutoonekana kwenye ziara hiyo ambayo Wabunge mbalimbali walishiriki.

Rais Magufuli akisalimia wananchi

Kwa mujibu wa Meseyeki waliompokea Rais walikosea kwa kutomkaribisha kiongozi huyo kwa mila na desturi za kimasai ambazo zimekuwa ni utambulisho wa Jimbo hilo.

"Ni kweli sikuwepo wakati Rais Magufuli anakuja Jimboni kwangu kwa sababu nilikuwa namuuguza mzazi wangu Dar es salaam, lakini kama ningeambiwa ningefika mapema sana'', amesema.

"Ningempokea vizuri kuliko wao walivyompokea, maana wamempokea kinyemela sana, sisi wamasai tuna utaratibu wetu wa kumpokea kiongozi mkubwa, ila sikufurahishwa walivyompokea Rais ningekuwepo tungempokea vizuri zaidi."

Akizungumza Desemba 2 mwaka huu Mbunge Viti Maalum Chama Cha Mapinduzi Amina Mollel bila kutaja jina alilalamikia kutokuwepo kwa Mbunge Jimbo la Arumeru Magharibi kwenye mkutano wa Rais Magufuli alipofanya ziara Jijini Arusha.

"Pale tulipokuwa sisi halikuwa jimbo la Nassari, lilikuwa jimbo la Arumeru Magharibi ambalo ni la Mbunge Gibson, sasa nashangaa watu wamenilisha maneno ambayo sikusema, sikumtaja Nassari wala mbunge wa jimbo japo ni kweli wote hawakuwepo kwenye mkutano," alisema Mollel