Alhamisi , 12th Mei , 2022

Baada ya Baraza Kuu la CHADEMA kuunga mkono maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho kuwavua uanachama wanachama wake 19, wanachama hao wakiongozwa na aliyewahi kuwa mbunge wa Kawe Halima Mdee wameonesha kupinga uamuzi huo

Halima Mdee amesema hakukuwa na uhuru kwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho katika upigaji wa kura, huku akisema kuwa kilichofanyika ni uhuni.

Mdee hajaweka wazi kama kuna hatua nyingine watachukua baada ya maamuzi ya Baraza Kuu lakini amesisitiza kuwa hakukuwa na haki katika upigaji wa kura

Makada hao wamefukuzwa baada ya Bazara Kuu kubariki uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kuwafukuza ndani ya chama kwa kukubali kwenda kuapishwa na kuwa wabunge kinyume cha matakwa ya chama hicho.

Katika mkutano wa Baraza kuu Idadi ya wajumbe walikuwa ni 423, Waliokubalina na maamuzi ya Kamati ya kuwafukuza Uanachama ni 413 sawa 97.6% na wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati kuu ni 5 sawa na 1.2%

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema hatua inayofuata ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuandika barua ya kumtaarifu Spika wa Bunge kuhusu uamuzi uliofanywa na baraza kuu kwa hatua zaidi ikiwemo ya kutangazwa kuvuliwa ubunge.

Mrema amesema uamuzi huo wa Baraza Kuu ni wa mwisho ka ngazi ya Chama hicho na hakuna rufaa nyingine wanayoweza kukata