Jumanne , 6th Sep , 2022

Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa serikali haiwezi kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa undugu, urafiki ama kwa kujuana kwani shughuli za elimu zinahitajika kwa kila mtu na hivyo ni wajibu wa serikali kufanya kwa haki na uwajibikaji uliotukuka.

Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda

Kauli hiyo ameitoa wakati akitangaza kuanza kazi rasmi kwa timu ya watu watano ya kufuatilia utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 itakayoongozwa na Profesa Allan Mushi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, huku lengo ni kuhakikisha malalamiko yanayotolewa kuhusu Bodi ya Mikopo yanapatiwa ufumbuzi

"Na kwenye hili tunakaribisha watu watoe taarifa kwa sababu kama kuna mtoto wa Mkenda uliyesoma naye utakuwa unamjua baba yake ni nani na uwezo wake, halafu wewe unaona mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa," amesema Profesa Mkenda

Prof Mkenda amesema kuwa mtu yeyote ambaye ana wasiwasi na utoaji wa mikopo anakaribishwa ili aweze kuisaidia timu kufanya kazi yake kwa kuwa na taarifa zenye usahihi wa hali ya juu kutoka kwa wananchi husika.