Jumanne , 16th Feb , 2021

Mkandarasi anayejenga stendi kubwa ya mabasi ya kimataifa ya Ngangamfumini, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro yenye thamani ya bilioni 28, ametoa wiki moja kwa serikali imlipe fedha zake ambazo ni zaidi ya bilioni 1 anazodai kabla hajasimama kuendelea na ujenzi wa stendi hiyo.

Charles Shimilwa, Msimamizi wa ujenzi wa stendi hiyo kutoka kampuni ya CRJE East Africa,

Akizungumza na EATV hii leo Februari 16, 2021, msimamizi wa ujenzi wa jengo hilo kutoka kampuni ya CRJE East Africa, Charles Shimilwa, amesema kuwa mpaka sasa kampuni hiyo imeshindwa kuendelea na ujenzi kutokana na madeni wanayoidai serikali kwa kipindi kirefu hali iliyosababisha kupoteza ajira zaidi ya 100.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya fedha na utawala ambaye pia ni mstahiki Meya wa manispaa ya Moshi, Juma Raibu, amesema endapo mkandarasi huyo atasimamisha ujenzi wa jengo hilo serikali italazimika kumlipa fidia kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi huo na kuiomba serikali kulipa fedha hizo ili kukamilisha kwa wakati ujenzi wa stendi hiyo.

Naye Diwani wa kata ya Ngangamfuni inapojengwa stendi hiyo, Stuart Nathanael, amesema endapo mradi wa stendi hiyo utasimama utaathiri shughuli za uchumi katika kata hiyo na manispaa kukosa mapato na kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kulipa fedha hizo kwa haraka.