Jumamosi , 25th Jul , 2020

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Maalim Seif Hamad amesema kuwa marehemu Benjamin William Mkapa alikuwa kiongozi jasiri na hakujali maamuzi yake kama wengine hawatoyafurahia.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Maalim Seif Hamad

Akizungumza akiwa nyumbani kwa Mkapa Masaki Jijini Dar es salaam alipofika kutoa pole kwa familia leo Julai 25, 2020 amesema kuwa kiongozi huyo ni miongoni mwa watu walioshiriki na kusukuma kufanikiwa kwa maridhiano baada ya kutokea kwa mauaji Pemba mwaka 2001.

Amesema kuwa marehemu Mkapa alipenda kutumia kauli ya kuwa Tanzania si mali ya mtu, hivyo viongozi waliobaki wahakikishe wanamuenzi kwa vitendo.

"Alikuwa kiongozi imara, alipenda amani na maridhiano alihakikisha anasawazisha kila penye mgogoro. Pamoja na mengine ambayo hatukuyapenda ila naheshimu sana misimamo yake" amesema Maalim Seif.

Rais mstaafu Mkapa amefariki usiku wa kuamkia Julai 24, Jijini Dar es salaam na anatarajia kuagwa kwa siku tatu kuanzia Julai 26 hadi 28 katika uwanja wa taifa na Julai 29 atazikwa kijijini kwao Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara.