Ijumaa , 8th Jul , 2016

Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto nchini Tanzania imesema ukosefu wa huduma bora za uzazi kwa wanawake, umechangia kuongezeka kuzaliwa watoto wenye mtindio wa ubongo nchini.

Hayo yamebainishwa wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo madaktari kutoka nchi za Zambia, Zimbabwe, Sudan Kusini na Uganda wa kufanya matibabu kwa watoto wanaozaliwa na mtindio wa Ubongo pamoja na waliopata ajali.

Katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Elifuaraha Kesi ni mama wa mtoto Violata Mbawala mwenye umri wa miaka minne anasema mtoto wake amehangaika nae kupata matibabu kwa muda mrefu.

Kufuatia Hali hiyo, mbali na ajali zinasosababisha watoto kujeruhiwa Serikali inasema kumekuwa na sababu mbalimbali zinazochangia watoto kuwa na mtindio wa ubongo ikiwa ni pamoja na kutopata chanjo ya polio kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Dkt. Othman Kiloloma akizungumzia hali hiyo anasema ajali zinazosababishwa na bodaboda nazo zimechangia ongezeko la watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji.

Mafunzo hayo ni ushirikiano baina ya Tanzania na Madaktari bingwa wa Upasuaji 12 kutoka nchini Uturuki.