Moto kwenye maduka jengo la UWT CCM Mkoa wa Njombe
Moto huo umetokea majira ya saa 3:00 usiku wa Aprili 1 mwaka huu ambapo mkaguzi Loti Madauda Kwa niaba ya Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Njombe amesema walipata taarifa ya moto huo majira ya 3:28 na kufika saa 3:31 na kuanza zoezi la uzimaji moto huo mpaka majira ya saa saba usiku.
Madauda amesema wamefanikiwa kuokoa vyumba 89 vya maduka ya wafanyabiashara hao na 21 zikiathirika na moto huo.
Aidha katibu Tawala Wilaya ya Njombe Emmanuel George amesema chanzo cha awali cha moto huo ni hitilafu ya umeme huku uchunguzi wa kina ukiendelea kufanyika na kisha itatolewa taarifa zaidi.
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara waliounguliwa maduka yao kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati tathmini ikiendelea kufanyika, kwani ni mara ya pili au ya tatu maduka yanaungua moto mkoani Njombe.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Njombe Julius Peter amelipongeza jeshi la zimamoto na uokoaji pamoja na wananchi kwa kujitokeza kuzima moto huo pamoja na kuokoa mali mbalimbali za wafanyabiashara huku akiwaomba wafanyabiashara kutulia wakati tathmini ya maafa itakapofanyika.




