Jumapili , 15th Nov , 2020

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii),Dkt. John Jingu amesema kazi ya kulea watoto inayofanywa na vituo vya kulelea watoto si kazi rahisi.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii),Dkt. John Jingu akiwa amembeba mmoja wa watoto katika kituo cha Kulelea Watoto wadogo cha Mgolole

Dkt. Jingu ameyasema hayo Mjini Morogoro wakati alipotembelea Kituo cha Kulelea Watoto wadogo cha Mgolole kinachoendeshwa na Kanisa Katoliki ambapo amevipongeza vituo vinavyohusika na malezi kwa watoto kutokana na kazi kubwa wanayoifanya kwa taifa.

"Kazi mnayoifanya ya kulea watoto si kazi rahisi , mna watoto kama 52 sio kazi rahisi unaweza ukakuta familia moja ina watoto watatu tu lakini suala la malezi linakuwa gumu ila ninyi mna watoto 52 na mnaweza. Hili mnalolifanya ni ibada katika Imani zetu zote na ninawapongenza sana kwa hili” amesema Dkt. Jingu

Aidha Dkt. Jingu amefafanua kuwa suala la malezi ni muhimu sana katika kuhakikisha tunajenga taifa lenye watu wenye maadili na uzalendo kwa nchi yao huku akisisitiza kuwa vituo hivyo lazima visajiliwe ili kutambulika na serikali na wadau wengine ili viweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri.