Ijumaa , 4th Dec , 2015

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally amesema wilaya yake imeshaanza kutekeleza agizo la usafi Desemba 9 kuanzia Desemba 2 mwaka huu wa kufanya ukaguzi katika nyumba za kulala wageni, hoteli na mama lishe.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally

Akizungumza na East Africa Radio, Fatma amesema zoezi hilo linaendelea huku tayari ameshatoa maagizo kwa watendaji wa vijiji na mitaa kusimamia usafi wa mazingira kwa wananchi wote katika ngazi ya kaya zao.

Aidha, amesema katika siku ya kilele cha shughuli hiyo ya Desemba 9, usafi wa mazingira utafanywa katika maeneo kadhaa ambayo ni maalumu huku wakianza katika eneo linalozunguka mnara wa Mashujaa.

Katika hatua nyingine uongozi wa zahanati ya kata ya Shangani, manispaa ya Mtwara Mikindani umeingia makubaliano ya kupokea fedha kutoka kampuni ya utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta (BG) kwa ajili ya kununulia vifaa tiba vya magonjwa ya dharura.

Katika mkataba uliosainiwa leo mbele ya mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally na mganga mkuu wa mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa, katika Zahanati hiyo, BG watakabidhi dola za kimarekani 280,000 ambazo ni zaidi ya sh. milioni 600.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Mkuu wa Ayfa, Usalama, Ulinzi na Mazingira wa BG-Tanzania, Stevenson Murray, amezitaja baadhi ya vifaa vitakavyopatikana kutokana na msaada huo kuwa ni pamoja na Gari la wagonjwa (Ambulance) na vifaa vya huduma za afya za dharura zitakazozingatia ajali mbalimbali ikiwemo kung’atwa na nyoka.

Naye, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dengego, ameishukuru BG kwa kutoa msaada huo na kusema kuwa wamekua mstari wa mbele katika kusaidia jamii katika sekta zote muhimu.