Ijumaa , 20th Mei , 2022

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amethibitisha tukio la mwanamke kujeruhiwa kwa risasi leo maeneo ya Sinza Lion, na kusema imempata kwa bahati mbaya baada ya Askari kufyatua risasi juu kwa lengo la kuwatawanya wananchi waliokuwa wanampiga mwizi wa simu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 20, 2022, wakati akizungumza na East Africa TV & EA Radio Digital, ili kutoa ufafanuzi wa madai yaliyotolewa na mashuhuda wa tukio hilo kwa kusema kwamba mwanamke huyo aitwaye Mariam amejeruhiwa na polisi.

"Ni kweli tukio hilo limetokea na jeshi linaendelea kulifuatilia, lakini ni kwamba askari walifyatua risasi juu katika juhudi za kumuokoa mtuhumiwa na kwa bahati mbaya kuna mwanamke amejeruhiwa ingawa anaendelea vizuri," amesema Kamanda Muliro.

Aidha Kamanda Muliro akimzungumzia mwizi huyo amesema, "Huyo mtuhumiwa hatujamtambua kwa sababu hajaweza kuongea, alikuwa tayari amepigwa, hawezi kuongea, hivyo tunalichunguza tukio hilo".