
Simu ya mkononi
Lengo la serikali kuweka tozo hizo ambazo ziliitwa ni kodi za uzalendo zilikusudiwa kufanikisha upatikanaji wa maji vijijini, ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa barabara vijijini na uboreshaji wa huduma nyingine za jamii.
Julai 14, 2021, watanzania waliamka na kukutana na utaratibu mpya katika utumaji na utoaji wa fedha kwa wakala wa simu ya mkononi ambapo walianza kukatwa tozo kati ya shilingi 10 na shilingi 10,000 kulingana na ukubwa wa muamala.
Tozo hizo zilileta kelele nyingi sana mitandaoni, kwani makato yalikuwa ni makubwa ukilinganisha na vipato vya Watanzania, kilio ambacho kilisikika hadi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo alitoa maagizo kwamba tozo haziwezi kuondolewa lakini zitapunguzwa.
Agosti 31, 2021, serikali ilitangaza kupunguza viwango vya tozo mpya ya serikali kwa asilimia 30 huku watoa huduma ya mawasiliano ya simu nao wakiridhia kupunguza kwa asilimia 10 viwango vya tozo wanazotoza katika miamala ya kutuma na kutoa fedha.
Serikali kupitia Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, ilitangaza mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa kodi zilizopatikana kutokana na tozo za miamala, na kueleza jinsi ambavyo zitanufaisha sekta ya afya na elimu nchini.