Ijumaa , 12th Oct , 2018

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt Vincent Mashinji amesema kuwa hawezi kukubali kuwa mtumishi wa serikali kwa ajili ya kukwepa mgongano wa kimslahi lakini kama atapewa jukumu na Amiri Jeshi Mkuu Dkt John Pombe Magufuli lenye manufaa kwa nchi hawezi kukataa.

Akizungumza na www.eatv.tv ili kufahamu kama angeweza kurudi kuwa mtumishi wa Serikali kama historia yake inavyoonesha ambapo alikuwa moja ya madaktari waliofanya kazi kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Dkt Mashinji amesema,

 "Naweza kufanya kazi na Serikali lakini siwezi kuwa mwajiriwa wa serikali sasa hivi kwasababu nimeshajiingiza kwenye Dunia nyingine ikiwemo biashara. Ni vizuri vijana wengine wanaotafuta uzoefu wa kiutumishi wakarudi kwenye utumishi wa umma na wakapata uzoefu wa kiutendaji tukawaachia wakaitumikia nchi ".

"Lakini tunautaratibu wetu kama taifa, ikitokea Amiri Jeshi Mkuu anapokutuma kazi huwezi ukakataa, kama ikitokea kama nimetumwa kazi kama Taifa nitafanya na nitawajibika kufanya kazi kwa moyo mkunjufu na furaha", ameongeza.

"Lazima wananchi tutofautishe shughuli za kisiasa na shughuli za kitaifa ikitokea leo hii nikiteuliwa na Rais kuwa mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba ya taifa siwezi kukataa kwa sababu jambo hilo lina manufaa kitaifa".