Ijumaa , 1st Aug , 2014

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ameutaka Umoja wa Katiba ya wananchi UKAWA kurejea katika bunge la maalum la katiba ili kuendelea na mchakato wa katiba mpya.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete.

Kwa mujibu wa rais Kikwete, suala lao linaweza kumalizika ndani ya bunge hilo kwa mifumo waliojiwekea wakati wa kuanza kwa bunge hilo.

Akizungumza na Wananchi katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi Rais Kikwete amesema kuwa Madai ya umoja huo ni jambo linalojadilika ndani ya bunge hivyo ni vyema wakaweza kurejea bungeni ili kupata suluhu ya jambo hilo.

Aidha rais kikwete amewataka wajumbe hao wa bunge la katiba kukaa pamoja na vyama vingine Ikiwemo CCM ili kuleta maridhiano ya pamoja katika kupata muafaka wa kuwapatia wananchi katiba wanaoitaka na yenye manufaa kwa umma.

Hapo jana, wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA wamesisitiza kuwa hawatorejea katika Bunge maalum la Katiba, kwa madai kuwa viongozi hao wa dini hawazungumzii kejeli, matusi, ubaguzi unaofanywa na baadhi ya wabunge wa bunge hilo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mmoja wa wenyeviti wa UKAWA Prof. Ibrahim Lipumba amesema ili warejee bungeni kujadili rasimu ya Katiba ni lazima maoni ya wananchi yaheshimiwe pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM waliotoa kauli za ubaguzi, kejeli na matusi wachukuliwe hatua.

Naye Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Mhe Freeman Mbowe amesema kwa sasa hawapo tayari kurejea katika bunge hilo huku akishangazwa na kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa CCM licha ya kuwa katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ili kurejea katika Bunge maalum la Katiba kwa maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Mhe. James Mbatia amasema endapo mchakato wa Katiba mpya utakwama yafanyike marekebisho machache ya msingi katika Katiba ya sasa ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi