Jumanne , 11th Feb , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amemuagiza Waziri wa TAMISEMI Seleman Jafo, kuhakikisha anamuandikia barua ya kumfukuza kazi mfanyakazi wa Wizara hiyo aliyechana na kuitemea mate Quran Takatifu mkoani Morogoro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Februari 11, 2020, Jijini Dar es Salaam, wakati akiwahutubia wananchi wa Kigamboni muda mfupi tu mara baada ya kuzindua rasmi Wilaya hiyo na kusema kuwa Serikali haipo tayari kuwa na wafanyakazi wapumbavu.

"Juzi nilimsikia Mh Jafo mtu mmoja kule Kilosa alichana kitabu kitakatifu, nakushukuru umechukua hatua ya kumsimamisha kazi, lakini mimi namfukuza kazi moja kwa moja, ashinde kesi asishinde huyo si mfanyakazi wa Serikali hatuwezi tukakaa na wafanyakazi wapumbavu" amesema Rais Magufuli.

Februari 6, mwaka huu kulizuka taharuki baada ya kijana aitwaye Daniel Maleki, kuonekana akichana na kutemea mate kitabu hicho, ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro siku ya Februari 7, lilitangaza kumchukulia hatua kali na kumfikisha mahakamani.