Ijumaa , 10th Mei , 2024

Polisi nchini Zambia wameonya kuwa Rais wa zamani Edgar Lungu ana hatari ya kukamatwa na kushtakiwa kwa "kujihusisha na shughuli zinazovuruga amani na usalama wa umma".

Edgar Lungu, Rais wa Zamani Nchini Zambia Akitembea Kuzunguka Mji Mkuu wa Lusaka

Hii ni baada ya umati wa watu kumzunguka Bwana Lungu wakati akitembea kuzunguka mji mkuu wa Lusaka, siku ya Alhamisi kutathmini gharama kubwa za kufanya biashara katika mji huo. 

Bwana Lungu alisema "anashangazwa na jinsi bei za bidhaa zilivyokuwa juu" chini ya serikali ya Rais Hakainde Hichilema. Watu wengi walionekana wakimshangilia kiongozi huyo wa zamani wakati akitembea katika mitaa ya mji huo.

Polisi katika taarifa yao walisema Bw Lungu alisababisha "usumbufu mkubwa kwa trafiki" wakati wa ziara yake.
Msemaji wa polisi, Rae Hamoonga, alisema kuwa "Tunataka kusisitiza kwamba vitendo kama hivyo ni mkusanyiko usio halali na bila kujali hadhi ya zamani ya mtu kama mkuu wa nchi, kufuata sheria sio jambo la kujadiliwa," 

Alimtaka rais huyo wa zamani kujiendesha "ndani ya mipaka ya sheria na kujiepusha na vitendo vinavyovuruga amani na utulivu wa umma".

Bw Lungu ambaye alipoteza urais kwa Rais Hichilema mwaka 2021, ametangaza kurejea katika siasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026.