Jumatatu , 22nd Jun , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amezitaja sababu zilizopelekea kuwang'oa wote kwa pamoja viongozi wa Jiji la Arusha akiwemo RC, DC na DED ni kwa sababu wao walishindwa kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo, badala yake walikuwa na malumbano yasiyo na tija.

Kushoto ni Rais John Pombe Magufuli, katikati ni aliyewahi kuwa DC Arusha Gabriel Daqarro, na kulia ni aliyewahi kuwa RC Arusha Mrisho Gambo.

Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Juni 22, 2020, Ikulu ya Dar es Salaam, wakati akihutubia mara baada ya kumaliza kuwaapisha viongozi aliowateua na kusema kuwa viongozi wa Arusha walishindwa kuelewana kwa kipindi cha miaka miwili, licha ya kukubali utendaji wao wa kazi lakini walimuudhi.

"Mtakumbuka hivi karibuni Arusha ilibidi nitengue uteuzi wa wote niliowateua kuanzia RC,DC na DED, kwasababu katika kipindi cha miaka miwili walikua wanagombana tu, kila mmoja ni Boss, kila mmoja anatengeneza mizengwe ya mwenzake sikufurahishwa, walifanya kazi lakini waliniudhi kutokushirikiana na kufanya yale niliyowaagiza" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amesisitiza kuwa, "Wamekaa wanabishana na kuwacheleweshea wananchi wa Arusha kupata stendi nzuri, ndiyo maana nimesema wapumzike kwanza na hili liwe fundisho kwa viongozi niliowateua, lazima mkajenge element za kuvumiliana kama unataka kubishana na kugombana nenda kabisheni nyumbani kwako na mke wako".