Alhamisi , 18th Jul , 2019

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Damas Ndumbaro, leo Julai 18, amesema Serikali ya Tanzania na Uganda, zimedhamiria kushirikiana kwa dhati  katika masuala ya biashara, yenye mlengo wa kukuza uchumi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Damas Ndumbaro

Dkt Ndumbaro ameyabainisha hayo, wakati wa kutambulisha uwepo wa mkutano wa jukwaa la kwanza la biashara, kati ya Tanzania na Uganda, ambapo ameitaka Sekta binafsi, kuhakikisha inachangamkia fursa ya kuangalia ni kwa namna gani itapeleka walimu wa lugha ya Kiswahili Uganda.

''Biashara kati ya Tanzania na Uganda, imekuwa kutoka shilingi bilioni 178 mwaka 2015, hadi kufikia shilingi bilioni 358 mwaka 2018 hivyo, Sekta binafsi iangalie ni namna gani tutapeleka walimu wa Kiswahili kwenda kufundisha lugha hiyo nchini Uganda'' amesema Dkt Ndumbaro.

Aidha Serikali ya Tanzania na Uganda, zimekubaliana kuanzisha ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga, usafirishaji wa gesi pamoja na ujenzi wa reli, itakayorahisisha usafirishaji wa bidhaa kati ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.