Jumapili , 17th Aug , 2025

“Tupo bega kwa bega na taasisi za dini. Tutaratibu safari ya Hijja, tutafahamu idadi ya wanaokwenda na kuunga mkono mahitaji yao ili waweze kushiriki ibada hii tukufu,” amesema Mkalipa.

Serikali mkoani Mwanza imelitaka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani humo, kuendeleza ushirikiano na taasisi zake kuratibu safari za mahujaji wanaokwenda kuhiji mwaka huu wa 1447 Hijria, huku ikiahidi kusaidia  Waislamu  kuhakikisha wanatimiza nguzo hiyo muhimu ya dini yao.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, leo Agosti 17,2025, wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Hijja lililofanyika jijini Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiry Mkalipa, amesema Serikali ipo tayari kushirikiana kwa karibu na BAKWATA kuhakikisha waumini wa dini hiyo wanapata fursa ya kuhiji Makkah mwaka huu.

 “Tupo bega kwa bega na taasisi za dini. Tutaratibu safari ya Hijja, tutafahamu idadi ya wanaokwenda na kuunga mkono mahitaji yao ili waweze kushiriki ibada hii tukufu,” amesema Mkalipa.

Pia , serikali katika kongamano hilo, imetoa rai kwa waislamu kuwekeza katika elimu ya watoto wao ikiwemo elimu ya dini, ili kuimarisha msingi wa imani na kumfahamu Mwenyezi Mungu katika hatua za awali za maisha.  “Kama tunataka kizazi kinachomcha Mungu, hatuna budi kuwekeza katika elimu bora. Tuwaandae watoto wetu waifahamu misingi ya dini, waepuke njia za mkato na uongo unaoharibu jamii,” amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Akitoa salamu za BAKWATA, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, amesema mwaka huu wa 1447 Hijria, matarajio ni kuona idadi kubwa ya Waislamu wa Mwanza wakitimiza ibada ya Hijja, si tu kwa sababu ya uwezo wa kifedha, bali  maandalizi, mipango na mshikamano wa dhati.