Jumapili , 14th Jul , 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafunguliwa mashtaka wanaosambaza taarifa za uongo na za kutengeneza kuhusu matukio ya utekaji na kupotea watu ambayo yanachafua taswira ya Serikali.

Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara wakati akijibu maswali mbalimbali ya wananchi wa Kata ya Kisorya, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, kufuatia maswali ya mmoja wa wananchi, ambaye alimuhoji juu ya matukio ya kupotea kwa watu.

Katika mkutano huo mwananchi ambaye amefahamika kwa jina la Mnyaga Semba amemhoji Waziri Lugola juu ya namna Wizara yake imejipangaje kutokomeza matukio ya utekaji, ikiwemo tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari Azory Gwanda, ambalo kwa sasa linaendelea kujadiliwa mitandaoni.

Waziri Lugola amesema, "watu hao wanakaa mitandaoni asubuhi hadi jioni wakizusha matukio hayo machafu wakiwa na lengo la kupata umaarufu wa kisiasa kuichafua Serikali ya Rais John Magufuli na wananchi wake ambayo inafanya kazi nzuri kuiletea nchi maendeleo kwa kasi zaidi".

"Naagiza Jeshi la Polisi liwachukulie hatua, wote ambao wanajihusisha na uzushi huu"

Waziri Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kufanya mikutano ya hadhara akisikiliza kero za wananchi jimboni humo.