Jumapili , 6th Dec , 2015

Uongozi wa shirika la umeme nchini Tanzania TANESCO umewafukuza kazi wafanyakazi saba waandamizi wa shirika hilo

Uongozi wa shirika la umeme nchini Tanzania TANESCO umewafukuza kazi wafanyakazi saba waandamizi wa shirika hilo wakiwemo mameneja kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo vitendo vya wizi, kudai rushwa, ubadhirifu wa mali wa shirika hilo pamoja na kutoa lugha chafu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo mhandisi Felchesmi Mramba amesema uamuzi huo umechukuliwa ikiwa ni mpango endelevu wa shirika hilo kuimarisha nidhamu kwa wafanyakazi wake kutambua wajibu wao wa kutoa huduma ya nishati kwa wananchi na sio kuwasumbua wateja.

Ametaja vitengo ambavyo wafanyakazi hao wamefukuzwa kuwa ni pamoja na ngazi ya mameneja, wahandisi na wahasibu katika mikoa ya Kinondoni Kaskazini, Katavi , Kagera na Ilala.

Hata hivyo Mramba ametoa siku saba kwa wateja ambao wanahujumu shirika hilo kwa kujiunganishia umeme kwa wizi kujisalimisha wao wenyewe kutokana na kuanza oparesheni maalumu ya nyumba kwa nyumba ya kuhakiki mita ili kubaini upotevu wa nishati ya umeme unaotumika bila kulipiwa.

Katika hatua nyingine mkurugenzi huyo amewataka wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini wasikubali kutoa zaidi ya sh. 27,000 wakati wa kuanganishiwa umeme wa REA, na endapo wataombwa kufanya hivyo basi watoe taarifa.