Ijumaa , 29th Jul , 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ujenzi Tanzania -TBA kuhakikisha wanakamilisha haraka miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma zinazojengwa nchini kote.

Ameyasema hayo mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi 851 zilizopo eneo la Bunju "B" ambazo zipo katika mpango wa wakala wa kujenga nyumba 10,000 kwa ajili ya watumishi wa umma na kuona hatua zilizofikiwa.

Waziri Mbarawa amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutawawezesha watumishi wa umma kupata makazi yaliyo bora na ya uhakika na hivyo kuiwezesha TBA kujipatia marejesho ya fedha walizowekeza kwa wakati.

Professa Mbarawa amewataka TBA kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa miradi ya nyumba na majengo nchini kwa wakati na kuziuza nyumba hizo haraka iwezekanavyo ili TBA iweze kupata faida itakayowawezesha kujenga nyumba nyingine badala ya kuwa na miradi mingi ya ujenzi ambayo haijakamilika.

Aidha Professa Mbarawa, ameitaka TBA kubadilika kimtazamo na kitaalamu kuanzia watendaji hadi wafanyakazi wake na kuanza kufanya kazi kwa malengo ili kuwezesha kukabiliana na ushindani wa kibiashara wa majengo hapa nchini.

Naye Mtendaji Mkuu wa TBA Mhandisi Elius Mwakalinga amemhakikishia waziri kuwa wakala wake utafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati mradi huo kwa kuwa inayo uwezo wa kiteknolojia wa ujenzi wa miradi ya majengo hapa nchini.