Ijumaa , 3rd Mar , 2023

Kufuatia uwepo wa matumizi ya vifaa vya afya visivyo na ubora Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba Nchini TMDA imeendesha zoezi la Utoaji Elimu kwa watoa huduma ya Afya ili kuvibaini vifaa tiba ambavyo havikidhi vigezo au vimekaribia kuisha muda wake ili kutoa taarifa kwa mamlaka.

Mamlaka hiyo imesema kuwa baada ya kufanya ukaguzi wa vifaa hupelekwa katika vituo vya afya kwaajili ya matumizi, lakini baadaye vingine huwa na dosari ambazo hubainika pindi zinapoanza kutumika.

Kaimu Meneja Ufuatiliaji Usalama TMDA Mary Masanja, akiongoza zoezi hilo katika Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam amesema kuwa mrejesho wa haraka kutoka kwa watoa huduma utaipunguzia mzigo Serikali ikiwemo kuingia hasara ya upotevu wa fedha.

Kwa upande wake Mfamasia kutoka Manispaa ya Kigamboni, Margreth Lali amesema elimu hiyo itawasaidia watumishi wa afya kufanya ufuatiliaji wa wananchi pindi wanapotoa huduma ili kubaini madhara wanayokutana nayo wananchi.