Alhamisi , 6th Oct , 2016

Wadau wa sekta binafsi nchini wamekutana jijini Dar es Salaam leo kujadili namna watakavyoshirikiana na serikali kuharakisha mpango wa ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Katika majadiliano hayo, suala la uhaba wa nishati ya uhakika pamoja na ukosefu wa rasilimali watu vimetajwa kuwa ni baadhi ya changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa haraka wa mpango huo.

Wakizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), wadau hao akiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini - CEO round table, Balozi Ali Mufuruki, amesema matarajio ya nishati yaliyopo hayaendani na ukubwa wa nishati inayohitajika kuendesha viwanda tarajiwa.

Serikali kwa upande wake imesema kila kitu kipo kwenye mwelekeo mzuri ambapo tayari kuna baadhi ya makampuni ya nje yameonesha nia ya kujenga viwanda nchini huku rekodi zikionesha kuwa tangu serikali ya awamu ya tano iingine madarakani takribani leseni 114 zimetolewa kwa ajili ya miradi mipya ya viwanda.