Jumanne , 4th Mei , 2021

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa mualiko rasmi kwa Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania  yatakayofanyika mwezi Desemba mwaka huu.

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.

Rais Samia ametoa mualiko huu rasmi wakati akihitimisha hotuba yake mbele ya viongozi na  waandishi habari nchini Kenya, akiwa katika ziara yake aliyoanza leo nchini humo ambapo ameahidi kuwa Tanzania itakuja kwa kasi kuwekeza nchini Kenya ili kukuza ujazo wa biashara.

Awali Rais Samia amesema nchi za Kenya na Tanzania zimekubaliana kushughulikia vikwazo vilivyopo hususan visivyo vya kodi katika mipaka ya nchi hizo mbili ili  kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo.

“Kwa lengo la kukuza biashara na uwekezaji kati yetu tumekubaliana kuendelea kushughulikia baadhi ya changamoto hususan  vikwazo visivyo vya kodi ambavyo vinatokea katika mipaka yetu, Tumekubaliana kuwa Mawaziri wetu wa Afya kukaa na kuangalia namna ya kurahisisha mfumo wa kuingia na kupimwa haraka watu wetu kwenye mipaka katika masuala haya yaliyoingia ya Covid 19, ili waweze kupita na biashara ziendelee'',” amesema Rais Samia

Naye Rais Uhuru Kenyatta ameeleza kufurahishwa na ujio wa Rais Samia huku akisema makubaliano yao katika kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili yatasaidia kukuza  na kutanua wigo wa biashara.

“Mawaziri wetu wameambiwa wahakikishe wanakutana mara kwa mara ili kuzingatia uhusiano wetu na kutatua shida ndogondogo miongoni mwa wananchi, suala la mahusiano tutaendelea kuyaimarisha kutoka safari za ndege, za reli na za kupitia baharini, kule upande wa kanda ya ziwa,” amesema Rais Uhuru Kenyatta