Jumanne , 10th Dec , 2019

Mkoa wa Dodoma umetekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt John Pombe Magufuli, la kuwaachia kwa msamaha wafungwa 385, kutoka katika magereza 6 yaliyopo mkoani humo.

Rais Magufuli

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa huo Dkt Binilith Mahenge akiwa katika Gereza la Isanga, amewataka wafungwa hao kwenda kuwa raia wema wanaozingatia, taratibu na Katiba ya nchi na kufanyia kazi ujuzi waliopatiwa gerezani.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma ACP Keneth Mwambije, amesema wafungwa hao wanatoka katika Gereza la Isanga, Kongwa, Msalato, Kondoa, Mpwapwa na King'ang'a, ambapo tayari wamepewa mafunzo mbalimbali ya ujenzi.

Mafunzo mengine waliyopewa wafunguwa hao ni Kilimo, kazi za mkono kama ufumaji wa vitambaa na vikapu.

Abdallah Ramadhani, aliyefungwa miaka 30 kwa kosa la ubakaji, amesema amejirekebisha na kuahidi kwenda kuwa raia wema.