Jumamosi , 29th Aug , 2015

Chama Cha Demokrasi na Maendeleo kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) leo kimezindua rasmi kampeni za urais ambapo uzinduzi huo umeshuhudia umati wa watu wakijitokeza.

Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA akiwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, Mh. Edward Lowassa

Akiongea katika mkutano huo Mgombea urais kupitia Umoja huo Mh. Edward Lowassa amesema kuwa wananchi watakapompa ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ataendesha mchakamchaka wa mabadiliko katika sekta zote.

Mh. Lowassa amesema kuwa ataweka vipaumbele katika sekta ya viwanda pamoja na kuboresha sera ya elimu ambayo ndio chachu ya mabadiliko katika kujenga uchumi wa nchi yoyote duniani.

Kwa upande wake mgombea mwenza Juma Duni Haji amesema kuwa watanzania wametaabika kwa muda mrefu bila kupata utatuzi wa matatizo yao ikiwemo maisha bora ila kwa serikali itakayoundwa na Mh. Lowassa itajenga mazingira bora kwa kila mtanzania.

Naye waziri mkuu mstaafu wa awamu ya tatu Mh. Fredrick Sumaye amesema kuwa ufisadi unaofanyika ndani ya Chama cha Mapinduzi ni mkubwa na wao kwa nafasi zao walikuwa wanashindwa kufanya maamuzi kutokana na mfumo uliokuwepo ndani ya chama hicho.

Aidha Mh. Sumaye amefafanua kashfa zinazotokea nchini Tanzania nyingine ni mpango wa kutengeneza kuwachafua baadhi ya watu kwa kuwa chama hicho kina mgawanyiko mkubwa ambapo watu wenye msimamo wanachafuliwa ili wasipate nafasi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA Mh. Freeman Mbowe amesema kuwa wamemchagua lowassa kuongoza mabadiliko kwa kuwa ni mtu ambae anauwezo wa kuamua na kuwatumikia wananchi.