Jumatano , 3rd Feb , 2016

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limezindua ombi la dola Milioni Tisa kusaidia kudhibiti kuenea kwa virusi vya Zika hususan Amerika ya kusini ambako virusi vimeenea katika takribani nchi 25.

Msemaji wa UNICEF Geneva, Christophe Boulierac

UNICEF imesema nchini Brazil, tayari inashirikiana na wadau na jamii kutuma ujumbe wa hamasa jinsi ya kuepuka kung'atwa na mbu na kutokomeza masalia ya wadudu hao na fedha hizo zitasaidia kupunguza makali ya madhara yake kwa watoto wachanga , familia na ukanda mzima wa Amerika ya Kusini.

Msemaji wa UNICEF Geneva, Christopher Boulierac amewaeleza waandishi wa habari kuwa UNICEF imesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua haraka na kuwapatia wanawake na wajawazito taarifa sahihi wanazohitaji ili kujikinga wao na watoto wao na pia kushirisha jamii jinsi ya kudhibiti kuenea kwa mbu anayebeba virusi hivyo.

Wakati huo huo WHO imesisitiza kuwa virusi vya Zika si tishio katika ujauzito kama HIV au Ebola lakini athari zake zina madhara makubwa sana kwa familia.