Ijumaa , 3rd Mar , 2023

Mamlaka ya Tunisia imepiga marufuku maandamano ya upinzani ambayo yalitarajiwa kufanyika siku ya Jumapili wiki hii. Wanachama wa muungano wa upinzani ambao wameratibu muungano huo wameyuhumiwa kufanya uhalifu dhidi ya serikalI.

Afisa mmoja wa Tunisia amesema ombi la muungano huo kuhusu maandamano hayo halijaidhinishwa na kwamba  baadhi ya viongozi wake wanashukiwa kupanga njama dhidi ya usalama wa taifa.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, mamlaka za serikali  zimeanzisha wimbi la kukamatwa kwa watu muhimu wakiwemo wapinzani na wakosoaji wa Rais Kais Saied, huku makumi yao wakishikiliwa.

Siku ya Alhamisi, polisi waliwakamata Sadok Chourou na Habib Ellouz ambao ni  maafisa wawili wakuu wa chama kikuu cha upinzani cha ennahda.  Chama hicho kimesema kukamatwa kwa watu hao kunalenga kutisha upinzani na kutoa wito kwa Watunisia kujiunga na maandamano yaliyopangwa.

Nchi hiyo imekuwa katika mzozo mkubwa wa kisiasa na kiuchumi, huku kukiwa na maandamano ya Watunisia waliokatishwa tamaa na uchumi na kupinga mamlaka ya karibu ya Bw Saied. Mnamo 2021, Bw Saied alifunga bunge na kubadili aina ya utawala kwa amri kabla ya kuandika upya katiba ya Tunisia.