.jpeg?itok=-rJ1H85X×tamp=1665415924)
Dkt. Bernadetha Rushahu, Mkuu Kitengo cha Ushauri na Unasihi UDSM.
Ikiwa leo Oktoba 10 ni siku ya afya ya akili ulimwenguni, hali ya jamii si shwari; maasi, mauaji na matukio lukuki yanayohusishwa na matatizo ya afya ya akili yamashika kasi, Dkt. Bernadetha Rushahu ni Mkuu Kitengo cha Ushauri na Unasihi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kila dakika moja angalau mtu mmoja hufariki duniani kutokana na matatizo ya akili na kuomba watu kuwa wawazi wa matatizo yanayowasibu ili kujiweka sawa kiakili.
“Kwakweli tatizo ni kubwa sana, kikubwa kinachohitajika ni elimu, watu wakishapata elimu ya uelewa kuhusu masuala haya basi tutaweza kupunguza matukio yanayohusiana na tatizo la afya ya akili. Lakini kingine cha mhimu ni kushirikishana, kwamba mtu unapokuwa na tatizo fulani kama mawazo au sonona au mtu kakuudhi shirikisha mtu wa karibu kuliko kukaa nalo Moyoni. Mtafute mwanasaikolojia akisaidie kumaliza changamoto yako kwa ushauri"- Bernadetha Rushahu, Mkuu Kitengo cha Ushauri na Unasihi UDSM.
Aidha, Daktari bingwa wa afya ya akili kutoka shirika la afya duniani Dkt. Alphonsina Nanai amesema kuwa ni vema ulimwengu mzima ukalichukulia suala la afya ya akili kama suala la ulimwengu na kulipatia kipaumbele zaidi, huku Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kwa Tanzania akisisitiza kwamba hakuna afya bila afya ya akili.
“Hivi sasa tunapozungumzia afya ya akili imekuwa ni tatizo kubwa, hadi sasa hivi kati ya watu 100 watu 26 wanakadiriwa kuwa na tatizo la afya ya akili na ndiyo maana maasi katika jamii yameongezeke. Hivyo nitoe wito kwa jamii kulichukulia kama tatizo la kidunia na lipewe kipaumbele ili kulimaliza, tusipofanya hivyo jamii inapotea"- Dkt. Alphonsina Nanai, Mtaalam wa Afya ya Akili WHO.