Ijumaa , 7th Oct , 2016

Serikali ya Tanzania inajipanga kuhakikisha vituo vyote vya afya nchini Tanzania kuanzia ngazi ya zahanati na wilaya zinakuwa na maabara ili kuwezesha upatikanaji wa matibabu ya uhakika.

Dkt. Hamis Kigwangalla

Mpango huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Khamisi Kingwangala, jijini Dar es salaam wakati akifunga kongamano la 30 lililoshirikisha watafiti wanasayansi kutoka nchi 17 ambapo amesema ni lazima maabara ziwepo kwenye kila kituo cha afya kwa mujibu wa sera ya afya inavyoagiza.

Kigwangalla amesema utoaji wa huduma za afya bila kuwepo kwa majibu ya vipimo vya uhakika vya wagonjwa ni sawa na ubabaishaji na kuchezea afya za watanzania hivyo maabara ni moja ya kipaumbele chake na atasimamia kuhakikisha uchunguzi wa afya za watanzania unakuwa wa uhakika.

“Mimi kama Daktari natambua umuhimu wa kuchukua vipimo vya kimaabara ambavyo vinatoa ushahidi wa aina gani ya matibabu yanamfaa mgonjwa,. Nitalisimamia hili kuhakikisha linatekelezeka kama ambavyo nahitaji kuwepo kwa vyumba vya upasuaji kwenye hosptali zetu” amesema

Wanasayansi watafiti wametoa mapendekezo sita kwa serikali kuhakikisha inayatekeleza kikamilifu ili kuboresha huduma na hali za afya kwa wananchi wake ambapo Mhe. Kigwangalla ameahidi kuwa mapendekezo hayo yatashugulikiwa.

Dkt. Kigwangala ametaja mapendekezo hayo kuwa ni pamoja na, kuanzisha kitengo cha udhibiti wa magonjwa ya mifupa, udhibiti wa magonjwa sugu yasiyo ambukiza, kuongeza juhudi za kuwawezesha watafiti na kuwajengea uwezo wanasayansi nchini, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ambavyo wanaweza kuhifadhi vyakula, kuandaa chakula na lishe.

Kigwangala amewahakikishia watafiti hao kuwa, serikali inatambua umuhimu wa tafiti za kisayansi ambazo kwa kiasi kikubwa hutumiwa na serikali katika utungaji wa sera na kutatua changamoto za afya na masuala mengine katika jamii hivyo kuahidi kusapoti shughuli za kisayansi.