Jumanne , 21st Jan , 2020

Wafanyabiashara na wakandarasi wa ndani Mkoa wa Katavi wamezitupia lawama halmashauri za mkoa huo kwa kushindwa kuwalipa madeni yao wanayodai kwa mda mrefu, hali inayopelekea baadhi yao kufilisiwa.

Moja ya kifaa cha ujenzi

Wamesema kuwa hali hiyo imewafanya kufilisiwa na mabenki, kuuzwa nyumba zao kwa kushindwa kurejesha mikopo na wengine kufunga biashara zao kwa kukosa mitaji.

Hayo yamebainishwa hii leo, Januari 21 katika kikao ambacho kimeandaliwa na Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo katika kazi hasa wanazofanya na serikali.

Lakini pia wakandarasi hao wamelalamikia kitendo cha mrundikano wa ushuru jambo ambalo linawakwamisha katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Juma Homera ametoa siku saba kwa wakandarasi wanaodai fedha zao kufika ofisini kwake na hesabu kamili ya madai yake kila mmoja na halmashauri husika kuhakikisha zinalipa madeni hayo kwa haraka.