Alhamisi , 25th Feb , 2016

Wanafunzi 46 wa Shule ya Sheria nchini Tanzania jana wamefika katika wizara ya Katiba na Sheria kushinikizo kupatiwa mikopo kutoka bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ili waweze kukabiliana na mahitaji pamoja na kujikimu.

Moja ya Majengo yanayopatika katika shule ya sheria nchini Tanzania (Law School).

Akizungumza mara baada ya kutoka katika ofisi hiyo, mwenyekiti wa wanafunzi hao Wellwel Steven amesema kuwa wamekuwa wakiishi kwa kubahatisha shuleni hapo baada ya bodi kubadilisha mfumo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi hao.

Bw. Steven amesema kuwa utaratibu wa awali ulikuwa ni kwamba wakiingia katika shule hiyo ya sheria walikuwa wakipewa ruzuku ya kujikimu wenyewe lakini baada ya kuingia wao ambao ni court ya 20 walibadilishwa kuingia kwenye mfumo wa kunufaika na mikopo ya elimu ya juu.

Aidha mwenyekiti huyo amesema kuwa baada ya kubadilishwa kwa mfumo huo wengi wameonekana hawana vigezo vya kupata mikopo hiyo, hivyo wamefika katika ofisi hiyo kwa kuwa wengi wao wameathirika na mfumo huo ambao zamani walikua wanapata ruzuku serikalini na sasa wanatakiwa kufikia vigezo ili kupata mikopo toka bodi ya mikopo ya elimu ya juu.

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo kaimu mkuu kitengo cha habari na mawasiliano Bi. Farida Khalfani amesema kuwa wanafunzi hao hawajafauta uratibu ambao wanatakiwa kufanya ikiwemo kukata rufaa ikiwa hawajapata mikopo lakini wao wamechukua jukumu la kufika moja kwa moja katika wizara hiyo.

Bi. Farida ameongeza kuwa wizara hiyo wala shule yenyewe ya sheria (Law School) haihusiki na utoaji wa mikopo hiyo, na kusema kuwa wizara iliingilia kati kuhusiana na utoaji wa ruzuku kipindi cha nyuma kwa kuwa sheria za mwanzo zilikuwa hazijaweka bayana juu ya upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi hao.