Jumatano , 20th Dec , 2017

Maafisa wa polisi nchini Zambia wamefutilia mbali mpango wa kuwaajiri raia wanane wa Kichina kuwa polisi nchini humo ndani ya saa 24 baada ya kuzindua mpango huo kufuatia pingamizi kutoka kwa raia.

Uamuzi huo wa kuwaajiri raia hao wa kigeni ulizua hisia kutoka kwa raia hususani kutokana na agizo jipya lililotolewa mapema mwaka huu ambalo linapiga marufuku maafisa wa polisi kuoa wageni kutokana na sababu za kiusalama.

Dickson Jere, ambaye ni wakili, alisema kuwa uteuzi huo ulikiuka katiba ambayo inasema wazi kuwa, Mzambia yeyote aliye na uraia wa nchi mbili hawezi kujiunga na idara za usalama.

Msemaji wa polisi nchini Zambia Esther Mwata-Katongo, alitetea uteuzi huo wa polisi akisema kuwa kabla ya wao kuteuliwa walichunguzwa na watafanya kazi chini ya usimamizi wa polisi wa kawaida.

Raia wa Zambia wenye uraia pacha pia hawaruhusiwi kujiunga na kikosi cha polisi.

Maafisa hao wapya walikuwa wamepewa jukumu la kupiga doria mjini Lusaka siku ya Jumatatu.