
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega
Ulega akiwa wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza ambapo wakati amefungua mafunzo rejea ya baadhi ya wataalamu wa mifugo amesema kuwa idadi ya wataalamu wa mifugo waliopo nchini kwa sasa haitoshelezi kila mfugaji kufikiwa na mtaalamu kwa wakati.
Amesema kutokana na ukuaji wa tekonolojia wafugaji wengi wanatumia simu za mkononi hivyo zikitumika vyema kwa kushirikiana na wataalamu wa mifugo itakuwa ni njia rahisi kwa wafugaji kutatuliwa changamoto zao kwa haraka zaidi na kupata ushauri wa ufugaji bora na kisasa
“Lazima wataalamu wetu muwe watumiaji wazuri wa hii mitandao ya kitaaluma ili kupeleka teknolojia kwa wafugaji wetu kwa kuwa hatuna uwezo wa kutosheleza wataalamu kila kijiji upungufu ni mkubwa.” Amesema Ulega
Aidha, amewataka wataalamu hao kuhakikisha wanajiwekea malengo kwa kuwa na wafugaji wachache kila baada ya muda ambao wanawafuatilia kwa karibu kuhakikisha wafugaji hao wanakuwa na maeneo yao wenyewe wanayoyamiliki na kuwapatia elimu na huduma bora za mifugo.
Amesema kwa kufanya hivyo wataalamu wa mifugo wataweza pia kuwafikia wafugaji ambao nao watatoa elimu kwa wenzao juu ya huduma bora za mifugo na kuwahamasisha kumiliki maeneo na kuwa na hatimiliki.