Jumanne , 20th Sep , 2022

Watu wawili wameuawa kikatili katika Kijiji cha Kidalimanda Kata ya Bunamhala Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu, huku chanzo cha mauaji hayo kikitajwa kuwa ni mgogoro wa ardhi wa muda mrefu

Akizungumzia tukio hilo la kijinai, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda, amesema kuwa mauaji hayo yamechochewa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na ameongeza shinikizo la watu kuheshimu sheria na haki ya mtu kuishi.

“Mnamo tarehe 9 mwezi wa 9,2022, majira ya saa 12 kuelekea saa 1 (ya jioni) katika Kijiji cha Kidalimanda Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu, Sinana Maduhu (48) na Maduhu Hilu (36) wote wakazi wa Kijiji cha Kidalimanda, walifariki Dunia baada ya kushambuliana na silaha za jadi. Kwamba, familia Masesa Njile, ilikwenda nyumbani kwa Sinana Maduhu na kuanza kuishambulia familia hiyo, kitendo kilichosababisha Sinana Maduhu kufariki Dunia papo hapo. Aidha, Maduhu Hilu alishambuliwa na Sinana Maduhu na yeye alifariki Dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Somanda,” amesema Kamanda Chatanda.

Kwa mujibu wa Kamanda Chatanda, watu wawili wametiwa nguvuni wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo la kijinai na watafikishwa mahakamani baada ya mafaili ya upelelezi kukusanywa na vyombo vya kiusalama.

“Chanzo cha tukio hili ni mgogoro wa shamba lenye ukubwa wa ekari moja, uliodumu kwa muda mrefu kati ya familia ya Masesa Njile na Sinana Maduhu. Aidha, mtuhumiwa Masesa Njile alifanikiwa kutoroka pamoja na familia yake na kutokomea kusikojulikana,” amefafanua RPC Chatanda.

Wakizungumza kwa sharti la kutokutajwa majina wala kurekodiwa, baadhi ya wananchi na ndugu wa marehemu wamesema kuwa, miezi kadhaa iliyopita marehemu Sinana Maduhu, alinusurika pia kuuawa baada ya kushambuliwa kwa mapanga na kuumizwa sehemu za mwili wake, na baadaye wahalifu hao walikwenda kumuomba msamaha kabla hawajarudi tena kumshambulia, katika tukio lililosababisha kupoteza maisha yake.

Uchunguzi umebaini kuwapo kwa taarifa za matukio ya kijinai katika Kijiji hicho cha Kidalimanda Wilaya hii Bariadi, ingawaje vyombo vya dola navyo vipo mguu sawa kuwanasa watu wanaojihusisha na uhalifu.